Monday, March 23, 2009

Dini usomi na kupotea kwa binadamu wa leo.

Mmarekani mmoja aliwahi kusema kwamba, binadamu wa sasa ameleta maendeleo na kufanya maajabu makubwa, lakini maendeleo hayo yaliyolenga kufanya dunia kuwa mahala bora pa kuishi (utadhani hapo mwanzo hapajawahi kuwa bora au paliumbwa kimakosa) sasa dunia imegeuka kuwa mahala hatari pa kuishi.

Angalia matatizo tuliyo nayo katika maisha ya Ulimwengu huu enzi zetu zimegeuka kuwa enzi za chuma wakati mwanzo palikuwa enzi za zahabu (iron and gold age).
Tuanzie katika uchafu wa mazingira kiasi kwamba badiliko la tabia nchi linatutishia na linatishia kila kiumbe hai, mimea, wanyama nakadhalika.

Tuje kwenye magonjwa hatari yasabibishwayo na dawa za kutibu magonjwa mengine, magonjwa yatokanayo na ’maendeleo’ ya binadamu wa leo kama vile salatani, ukimwi nk
Bila kusahau ukosefu wa chakula halisi na cha asili kilichotolewa na Nguvu kuu (MUNGU?) na sasa ni kula makemikali yanaonekana kuwa matamu mdomoni kumbe ni sumu mwilini.

Amani, umoja na mshikamano hakuna tena. Binadamu wa sasa amewekeza katika kupenda na kuthamini vitu vya duniani hata vile asivyovihitaji na sasa utu umeisha ni mali kwa kwenda mbele. Ni bora ufe ili jamaa apate pesa zake hata kama ni ndogo utadhani tunaweza kuishi peke yetu duniani kwa kukumbatia vitu au utajiri hata ule tusiouhitaji huku tukiwanyanyasa wenzetu.

Ukitembea sehemu zozote, hutakosa askari wenye siraha kali na hatari eti wanalinda usalama! Watu wananunua bastola ili kujilinda sijui dhidi ya nani, na mwisho wa yote zinawalipukia na kuwaua wao au jamaa zao mbao hata sio majambazi wala nini na wakati mwingine kuwapeleka kifungoni.

Viwanja vya michezo, ndege, kumbi za starehe nk, zimekuwa sasa ni za kuingia kwa kukaguliwa na mitambo maalumu ili kuzuia uharifu lakini wapi, bado kila kitu sasa kimekuwa ni saraha ya kujeruhi na kuuwa kama vile viti, meza, chupa za maji, bia na hata soda. Ikishindikana basi jamaa wanakojoa kwenye chupa za maji na kukurushia ili tu udhibitishiwe kuwa dunia si mahala salama pa kuishi

Vijana wamejiingiza katika uvutaji bangi, ulevi na madawa ya kulevya. Sigara na pombe ni halali kwa kila mtu. Eti serikali zinazuia uvutaji sigara, lakini unaruhusu matangazo ya kuvutia vijana wavute sigara yakiwa na kijisehemu kidogo kisichoonekana vizuri, kinachoonya juu ya hatari ya uvutaji sigara.

Pombe nayo ni kilevi hatari kinachouzwa hadharani. Serikali zinafurahia ulipaji kodi kwani zenyewe zinafurahia pesa na kutajirika fasta fasta bila kujali madhara. Ninauhakika kama wauzaji wa ’unga’ wangejiandalia njia nzuri za kulipa kodi, basi serikali za dunia hii zingeruhusu yauzwe yakiwa na nembo ya kuonya kuwa ni hatari.

Eti sasa tuna dini zenye lengo la kutuwezesha kukua kiroho na kutupeleka kwa Mungu, wakati ndo zinaleta ugigiri kati kati yetu. Kwanza kazi yake ni kusambaza woga juu ya uwezekano wa Mungu kutuchapa, kutuua na kututelekeza motoni, utadhani wesemayo hayo wanamfahamu Mungu au wanaukaribu naye wa kutosha.

Viongozi wa dini wametumia nafasi zao kwa kuweka maagizo yao ili watafutao kukua kiroho wayafuate, kumbe hamna lolote. Mungu mwenye upendo, sasa amekuwa Mungu mwenye kutisha. Anamiliki moto, siraha kali na funguo za kuzimu, tayari kutudumbukiza humo! Kumbe yeye amejaa upedo tu anapenda kila kiumbe.

Baada ya dini kuwa zimekuja na ubaguzi wa kila moja kusema kwamba Mungu wake ni bora kuliko wa mwingine, sasa dini hizo zimechagua mataifa (yale zilikoanzia au yalikokuwa makao yake makuu) na kuyaita eti ni mataifa teule ya Mungu.

Kwa mfano upande wa wakristo, wao wanataifa la Israel eti ndo taifa teule la Mungu pekee duniani. Wanadhibitisha hilo eti kwa kuangalia mapigano ya kijinga na ya kinyama duniani kati ya israel na palestina eti waisrael wanashinda kwa sababu Mungu yupo nao.

Swali gumu na linaloonyesha upotofu hapa ni eti taifa teule la Mungu kazi yake ni kupigana, kuuwa na kushinda vita kwa kugombania tu ardhi? Je ni kuendelea kiteknolojia kwa kutengeneza siraha za kuulia watu wa Mungu? Eti ni kukua kiviwanda na kuharibu hali ya hewa ili binadamu na viumbe vingine viteketee bila makosa? Ni Mungu gani huyo? Huu ndio upendo wa Mungu kupitia taifa lake teule?

Hapa ndipo wanakuja wale wanaojiita wasomi na hoja zao za usomi wa kukubali kila akifanyacho mzungu kuwa ni sawa na sahihi wakati tukipeleka ulimwengu mahali pabaya na hatari. Hatuna watu wa kuangalia kwa makini na kufikiri kabla ya kutenda ila usomi wetu ni kuiga kila ujinga wa Mzungu.

Tuna wanasiasa wanaopenda sana na watu wao lakini kila mahali wanakuwa na ulinzi mkali, sasa wanapendwa na nani? Mlinzi anayewafuata futa na bunduki kila mahali au jamaa wanaotamani kuwachapa makofi na mateke? Eti wanabaraka za Mungu kuongozwa, japo wanalindwa vikali wakati Mungu na siraha hawafanani hata kidogo!

Kama nilivyomnukuu msemaji hapo mwanzo, alimalizia kwa kuonya kwamba, kamwe huwezi kumaliza matatizo kwa kutumia fikra zile zile ulizotumia kuyatengeneza. Na sasa ni lazima tubadilike, tuitafute kweli ili ituweke huru. Ni lazima turudi nyuma. Tuige maisha kama zilivyoishi jamii za kiafrika za enzi zile ili tuweze kuanza upya na kuishi kwa kuthaminiana na kupendana.

Naishia hapa lakini kumbuka akili zetu ni tunazojisifia nazo, zinatuongoza kufikiri upumbavu kuubariki na kuuishi. N i lazima tuishi kiroho zaidi badala ya kimwili, kiakili na kuongozwa na hisia

No comments: