Saturday, March 14, 2009

email kutoka kwa Fredi katawa

From: fred katawa
Subject: UTAPELI
To: mwafrikahalisijlkamala@yahoo.com
Date: Saturday, March 14, 2009, 4:37 AM

JE HII NI AINA MPYA YA UTAPELI?
Ni asubuhi ya alhamisi mojawapo ya mwezi huu wa tatu,nimeamka mapema naitizama siku naona kuwa ni njema kama zilivyo siku zingine.Nachukua kitabu changu kidogo na kuandika mambo nitakayoyafanya kwa siku hiyo
Kati ya mambo mengi ninayopanga kufanya siku hiyo,mojawapo ni kunyoa nywele na ndevu kwenye salon za hapa Bongo.
Saa tisa alasiri inanikuta nikiwa maeneo ya Biafra Kinondoni kandokando ya barabara ya Kawawa.Nikiwa natembea kwa miguu ghafla macho yangu yanaona neno ........SALON.Nakumbuka kuwa mojawapo ya mambo inayotakiwa nifanye kwa siku hiyo ni kunyoa nywele.
Naingia kwenye hiyo Salon.na kupokewa na hali ya ubaridi wa kiyoyozi.Kama ilivyo ada yangu naangalia bei ya huduma imeandikwa hivi,kunyoa nywele tsh 1000,nywele na ndevu tsh 2000.Nashtuka kidogo kwa kuwa nimezoea salon nyingi hapa Dar kunyoa nywele na ndevu ni tsh 1000.
Baada ya kuangalia mandhari ya salon hiyo inanivutia na ninaridhika kunyolewa kwa tsh 2000nikizingatia kuwa mfukoni nina tsh 10,000 naona haitaniathiri sana katika bajeti yangu ya siku hiyo.
Ninapoendelea kunyolewa naanza kuchunguza zaidi mandhari ya salon hiyo,naona kuna screen ikionyesha " Super sports" na kandokando kuna vikorombwezo kibao vya gharama kubwa.Kinachonishangaza zaidi ni simu walizonazo hawa vinyozi wasiopungua watano.Simu moja inagharimu kati ya tsh 400,000 na laki 600,000 ninajiuliza moyoni kwa kazi hii tu ya kunyoa nywele ndo inawafanya wamiliki vitu hivi?
Sauti ya kinyozi inanishtua "bro una mba wengi kichwani"ni kweli ninamjibu"kuna mafuta nitakupaka yatakusaidia sana"ananieleza,ninamshukuru ."naona usoni una chunusi "ninakubali,ananiambia anayo mafuta mazuri kwa chunusi kwa hiyo atanipaka pia,namshukuru tena kwa mara nyingine.
Baada ya kumaliza kuninyoa na kunipaka mafuta nampa noti ya tsh 10,000 anakwenda nje kutafuta chenji,anarudi na kunikabidhi tsh 2,000,ninamkumbusha kuwa nimempa tsh 10,000.Ananiambia kuwa gharama ya kunyoa ni tsh 2000 na kupaka mafuta ni tsh 6,000 ninapigwa na butwaa ninamuuliza kwanini hakunieleza mapema na ubaoni hazijaandikwa gharama za kupaka mafuta?Ananiambia kuwa alidhani ninajua kwa kuwa wote wanaoingia kwenye hiyo salon wanajua hilo.
Napanda daladala kuelekea kwangu,bajeti yangu imetibuliwa na mambo yameenda ndivyo sivyo.Ndani ya daladala ninajiuliza,JE HII NI AINA MPYA YA UTAPELI?
MR KAMALA TUNDIKA KWENYE GLOBU YAKO UKIPENDA,ILI WADAU WATUSAIDIE MAJIBU,KATAWA

7 comments:

Masangu Matondo Nzuzullima said...

Hata mimi haya yalitaka kunikuta. Nilikwenda kwenye salon moja pale Mikocheni. Ilikuwa salon nzuri sana - kila kitu mle ndani ni ghali mpaka nilidhani kwamba pengine hawa jamaa walikuwa na biashara nyingine pale (mf. unga). Nilikwenda nikiwa nimevaa kaptula, kandambili na kifulana na kwa hivyo sikupata mapokezi mazuri sana. Pengine walidhani kwamba siwezi kumudu kulipa hiyo 1800. Basi nikakaa kwenye kiti na jamaa akaninyoa. Alipomaliza akaniambia kwamba nilikuwa na kitu kinaitwa dandruff (kama sijakosea) na ilikuwa lazima anipake mafuta fulani yanayogharimu 7,000. Nilimwambia sina pesa kwani nilijua kwamba sikuwa na tatizo lolote. Basi niliambiwa niingie katika kijichumba kingine ambako nilimkuta binti mmoja aliyeniambia kwamba ili nisiende na nywele huko niendako basi ataniosha kichwa tena kwa sabuni maalumu. Nilipouliza bei nikaambiwa ni 3500. Nikasema hapana kwani nilikuwa siendi mbali na hapo. Basi nilitoka nikawapa noti ya sh. 10,000 na wakanirudishia chenji kamili huku wakiwa wamekasirikakasirika. Mlango unaofuata kulikuwa na mkahawa na niliingia pale nikaagiza ugali na sato mzima kwa sh. 4,800. Nikawaacha na dandruff zao. Ndiyo huu ni utapeli tena wa macho. Hayo mafuta aliyotaka kunipaka (siyo chupa nzima) hapa Marekani yanauzwa dola 4.36 Walmart. Ni ki-tube kikubwa ambacho pengine mtu unaweza kujipaka mara 20-40. Ukifanya mahesabu utaona kwamba jamaa wanatengeneza pesa si mchezo. Ni Bongo ati!

Shabani Kaluse said...

Hata Buguruni ipo Saluni ya aina hiyo, Tena kuna Mabinti wazuriiii, kama huwezi kudhibiti hisia zako za kuendeshwa na mwili basi umekwisha.

Mzee wa Changamoto said...

Sasa huo ni utapeli? Ni wizi. Wizi mkubwa maana hata hayo mafuta ya Shs 6000 si tiba kamili. Ni dozi moja ambayo sina hakika kama yanaweza kukuondolea m'ba wote.
Nadhani tapeli ni neno linalopunguza uhalisia wa wanalotenda.
HUO NI WIZI

kamala J Lutatinisibwa said...

tehe yaani hata mimi niliwahi kukutana nao pale saluni ya victoria na nilibakiza elfu tano nzima kwa kufanya mambo ysiyokuwa na umuhimu wala nini japo lengo langu lilikuwa ni kujifunza sikulalamika.

ila pole sana ndg katwa. ukiona saluni ina kyoyozi na sofa za bei juu ujue sio bure ni lazima uchunwe. iweje kinyozi amiliki gari la bei baya bila kufanya kautapekli kidogo walau?

fredkatawa said...

Nimejifunza mengi kumbe hata mikocheni na buguruni zipo!Kama alivyosema Mzee wa changamoto hawa ni wezi.Kamala na Nzuzulima kumbe nao yaliwakuta nae kaluse kumbe anawafahamu!

Nuru Shabani said...

Huo wizi umezagaa sana mjini hata mimi nakumbuka niliwahi kwenda kunyoa saluni moja kule kwetu tabata wakaniambia nina mba kichwani,watanipa dawa,nikauliza bei wakasema ni sh.4000/- nikawambia basi.Nilipotoka nipita duka la madawa nikaulizia kama wana dawa ya mba wakasema wanayo nikauliza shilingi ngapi wakaniambia ni 2500/- dozi nzima.Nikagundua hawa jamaa wanattengeneza sana pesa.

SIMON KITURURU said...

Hawa jamaa sitaki kusema hata ni shilingi ngapi walitaka kuniosha nywele mimi nisiye kata nywele !

Lakini sidhani au siwezi kuwaita kuwa ni wezi kama ni kitu kijulikanacho!:-(