Tuesday, May 12, 2009

kuchapa viboko, moja na moja ni moja,

haya ni maoni ya mwanakijiwe mchambuzi maarufu kama mpagani aliyeokoka......

Kamala, nilichapwa hizo fimbo nikingali mdogo (nyumbani) na zilizidi nilipoingia shule hadi darasa la sita!

Leo hii nakubaliana nawe kuwa hiyo tandikwa tandikwa sio njia ya kufundisha watoto wetu. Na hata kwa wafungwa nayo haisaidii!

Nimevutwa na hilo la mantiki ya hesabu (moja ongeza moja ni moja).

Mantiki hii nimeitumia katika makala moja, niliyokwisha andika...lakini bado kuchapishwa... kuhusu demokrasia yetu nchini.

Hususan, nimeitumia katika mkitadha wa kujaribu kusuluhisha au kutafuta muafaka miongoni mwa sehemu za Muungano (Tanzania Bara na Tanzania Visiwa)...Napenda kuiita Tanzania Visiwa na wala si Visiwani, kama vile tunavyoiita Tanzania Bara na wala si Tanzania Barani!

Kwahiyo, niruhusu niiendeleze hesabu hiyo, ki-siasa:

Akingali hai, Mwenyekiti wa CCM Mwalimu Julius Nyerere alilikemea kwa ukali pendekezo la kuunda federesheni na serikali zake tatu, yaani, Serikali ya Tanzania Bara, Serikali ya Tanzania Visiwa na Serikali ya Muungano.

Mwalimu Nyerere alidhihirisha kwa mantiki yake kwa hesabu za vitu-guswa (au vitu-onekana).

Ni hesabu ya mwanzo kabisa: moja ongeza moja ni mbili. Nyerere alikataa kata ya kukubali: moja ongeza moja ni tatu!

Mpaka sasa tunaamini kuwa jumla hiyo ya moja ongeza moja ni mbili ni kweli kila mara bila kujali mikitadha! Ndio maana hata Mwalimu Nyerere alikazania kuwepo kwa serikali mbili tu.

Mimi binafsi si mtaalamu wa hesabu – somo lililokuwa likinipa ushindi wa chini shuleni.

Naafiki na Mwalimu Nyerere kwa dhati kwamba katika mikitadha ya hesabu/nambari za vitu-guswa au vitu-onekana viwili: moja ongeza moja ni mbili.

Lakini si kweli hata kidogo katika mikitadha mingine!

Kwahiyo, ninahitilafiana na Mwalimu Nyerere kwa kufikiria kuwa Tanganyika na Zanzibar ni vitu-guswa au vitu-onekana!

Tanganyika na Zanzibar sio chungwa au embe, ambayo chungwa moja ongeza chungwa moja ni machungwa mawili ua embe moja ongeza embe moja ni maembe mawili!

Tanganyika na Zanzibar ni ideas. Na mantiki yake ni ya moja ongeza moja ni moja!

Na hii iko sawa pia kwa vitu-onekana vyenye uwezekano wa kuunganishwa, kwa mfano, majumba. Majumba mawili yakiunganishwa, linakuwa ni jumba moja tu kubwa).

Nitatoa mifano miwili kudhihirisha mantiki hii ya moja ongeza moja ni moja kutoka katika Biblia. Mifano hii ni kati ya vitovu vya imani ya wa-Kristu:

Mfano 1: Mwanzo 2:24 na Marko 10:7 tunaambiwa kuwa mwanaume na mwanamke wakioana wanatekeleza idea ya ndoa inayovuka mikitadha ya vitu-guswa au vitu-onekana viwili (mwanaume na mwanamke)!

Cha maana kinakuwa ni ndoa; ni mkataba. Na mkataba wa ndoa, kama ilivyo mkataba wowote, hauvunjwi hovyo hovyo! Wawili hao wanafikiriwa kuwa kitu kimoja.

Kwahiyo, tunaweza kutamati kuwa ndoa ya ki-Biblia inauminisha kuwa moja ongeza moja ni moja!

Kwa waliooana, kama kila mmoja atajiona kwamba moja ongeza moja ni mbili, basi mtafaruki utaanza na kuleteleza kutengana, kuachana na kuvunjika kabisa kwa ndoa yenyewe, hatimaye.

Matokeo yake yatakuwa kwa hao wawili kubakia ya moja ongeza moja ni mbili!

Mfano 2: Kwa kifupi, imani ya ki-Biblia inawaasa waumini kuwa kuna Mungu mmoja tu ingawa kuna Mungu Baba, Mungu Mwana na Roho Mtakatifu (Utatu Mtakatifu).

Kwahiyo, mfano huu ni sawa na kusema moja ongeza moja, ongeza moja na ongeza moja ni moja na wala si tatu!

Tuingie ya kwetu hapa - ya ki-dunia - kwa kutoa mifano minne:

Mfano 1: Bila kujali ukubwa, eneo, uzito, ujazo, na kadhalika, tuangalie ya vimiminiko au dabwadabwa, kwa mifano, matone ya kahawa, lubisi, kangara, ulanzi, maji, maziwa, chai, asali au damu (hakuna cha ushirikina hapa), na kadhalika.

Ukidondosha tone moja la kahawa juu ya karatasi au chombo kingine, halafu uongeze tone la pili juu ya la kwanza, huwezi kuona matone mawili; utaona tone moja tu kubwa kwa vipimo vyake.

Na unaweza kuongeza tone la tatu au la nne huwezi kuona matone matatu au manne ya kahawa! Utaona tone moja tu kubwa kwa vipimo vyake!

Kwahiyo, kulingana na mkitadha huu, moja ongeza moja ni moja!

Mfano 2: Tuangalie mkitadha mwingine, u-rafiki.

Kama ilivyo ndoa niliyoitaja hapo juu, u-rafiki wa watu wawili (au zaidi) ni sawa na moja ongeza moja (hadi kufikia hiyo jumla ya nambari ya ma-rafiki) ni moja!

Kwahiyo, kiini cha u-rafiki ni moja!

Mfano 3: Tuangalie tena ya mikoa ya nchi yetu. Kama mikoa miwili ya Lindi na Mtwara ikiungana, itakuwa ni moja ongeza moja ni moja (mkoa mmoja mkubwa kwa vipimo vyake)!

Mfano 4: Tuangalie ya timu ya mpira wa futiboli (soka) au kandanda. Upande mmoja huchezwa na watu 11. Lakini hatusemi tumeingiza uwanjani wachezaji wetu 11; tunasema tumeingiza uwanjani timu moja.

Kwa mantiki hii hii, ili kuendeleza Muungano wetu wa nchi mbili huru za Tanganyika na Zanzibar zilizoamua kuungana (wa-Uingereza wanaita, to exercise a political marriage of convenience), tuuchukulie Muungano wetu kwa mifano ya ndoa, Utatu Mtakatifu, urafiki, jumba, mikoa, timu au matone mawili ya kahawa, lubisi, kangara, ulanzi, damu, maji, asali au soda bila kujali ukubwa au udogo wa kila tone!

Tukizingatia saizi, kwa mantiki hii hii, tone moja kubwa (Tanganyika) ongeza tone moja dogo (Zanzibar) ni tone moja kubwa zaidi (Tanzania)!

Mantiki hii inaweza kabisa kutusaidia kunasua a political marriage of inconvenience inayojining’iniza machoni petu, kuhusu Muungano wetu!

BAP

No comments: