Thursday, July 2, 2009

Tumesahau na kuacha kazi iliyotuleta duniani.


makala haya niliwahi kuyaandika katika jarida la rai.......

Binadamu kama viumbe vingine kaletwa duniani kwa sababu maalum ili kukamilisha kazi maalumu ambayo maumbile (Mungu?) yalimtuma kuja kuifanya hapa duniani. Ndio maana kuna watu wenye vipawa na uwezo tofauti tofauti katika mazingira yetu tunayoyaishi. Kila mtu katumwa kuja kuitenda kazi fulani na akiimaliza, arudi au aondoke.
Wengi tumepotea na kupotoka na kuingia kwenye vitu vingine. Tumevamia kazi za wengine na kuishi kwa kuongozwa na tamaa kwa kuvutiwa zaidi na anasa za dunia hii. Mwili wetu wa hisia kwa kushirikiana na akili zilizojazwa mawazo hasi kuliko yale ya chanya, ndio umekuwa kiongozi wetu. Tunapenda kujionyesha, kujisifu, kujisikia na hivyo tunatawaliwa na matatizo ya kihaiba (ego) zaidi kuliko uhalisia wetu.
Mtoto akishinda mtihani au akipelekwa shuleni, haruhusiwi kusomea kile anachokipenda bali hulazimishwa na wazazi kusomea kile kilichowashinda wao au chenye sifa ili waje kujisifu jinsi walivyokuwa na kijana msomi wa fani fulani nzuri hata kama yeye haipendi na hivyo kumpotezea lengo lake la kutimiza kile kilichomleta duniani kufanya.
Maisha yetu yanazidi kuwa ya hovyo yasiyo na msimamo wala mwelekeo, ni bora liende tu kama vile tulikuja duniani kwa bahati mbaya vile!
Wanasiasa na viongozi mbali mbali wapo kwenye nafasi walizonazo ili wapate wao mradi au kwa sababu kunalipa japo yawezekana hawapendi kufanya kazi wanazozifanya. Hata wewe unayesoma hapa yawezekana hupendi kazi yako, unaifanya basi tu kwa sababu ulilazimika kuisomea au upate pesa. Hakuna binadamu aliyekuja duniani kutafuta pesa bali pesa ni matokeo ya kufanya vyema kazi zetu na hasa zilizotuleta.
Ndio maana tunaishi na jamii yenye uchungu, visasi na hasira kwa sababu kila mtu anachukia kila hali na mazingira ya kazi yake kwa sababu hakupaswa kufanya kazi hizo.
Ukichukia kazi yako kwa kujua au kwa kutokujua, basi ujue unajichukia wewe mwenyewe na huwezi kujipenda. Ndio maana wanasiasa wanajiongezea pesa na wengine kukumbwa na kashifa kibao za rushwa, ni kwa sababu waliingia kwenye kazi hizo kwa tamaa ya fedha na sio kwa upendo wao au kazi zilizowaleta duniani.
Wazee wetu wakizeeka tunawatafutia vijikazi ili wazeekee pale, je unategemea ufanisi hapa ua kuboronga kama tunavyoona? Sasa tunakaa penmbeni hata majukumu yetu tunawalaumu wengine kwa kutokuyatimiliza. Tunategemea misaada kutoka kwa wahisani na tunailalamikia serikali na kuitukana utadhani sio serikali yetu kumbe suruhuisho la matatizo yetu yamo ndani mwetu!
Hatuna budi kujikagua na kutafuta ni wapi tulipoteleza na kurekebisha mara moja. Yatubidi kudadisi na kujua kazi zilizotuleta duniani ili tuishi vyema kwa furaha na kwa faida ya jamii pana. Ndio maana wasanii wa miziki ya kizazi kipya wanaimba nyimbo za kimapenzi tu. Kwa sababu wao hawajazaliwa kuimba hata kama wanasauti nzuri na hivyo wanaimba tu kwa sababu wamepata nafasi ya kuimba. Waigizaji wa filamu nao hawana jipya. Ukiangalia filamu zao hazifanani na mazingira ya ‘Bongo’ na hivyo kuigiza sio kazi yao, ni kwa sababu wamejikuta huko au mazingira yamewalazimisha kuingia huko au hawana jinsi.
Tafuta kazi yako na uifanye vyema. Kazi yako ya kwanza iliyokuleta duniani ni malengo. Wanasema maisha ni malengo na kwa hiyo lazima ujiwekee malengo ya msingi na kuyafuata. Nasema malengo ya msingi kwani malengo mengine hayana maana. Kama lengo lako ni kujilimbikizia pesa au kupata utajiri mwingi basi iwe ni kwa kufanya mambo ya msingi na sio kupitia njia za panya kama kuingia madarakani kwa kununua kura nk kwani kufanya hivyo kutakusababishia matatizo ya shutuma, tuhuma, malalamiko na laana.
Basi lengo letu kubwa liwe ni kujua vipawa vyetu na kazi zilizotuleta duniani ili tuishi vyema na kwa furaha. Kumbuka kuwa lengo ni jambo lolote lile ambalo katika kulitimiza kwako unakuwa na furaha na kwa hiyo kama unataka pesa lakini unafanya kazi usiyoipenda, ni bora kuachana nayo na kufanya ile uipendayo ili uwe na ufanisi na ubunifu katika kazi yako.
Utajua kazi iliyokuleta kwa kuifanya, kuifikiria au kuona wengine wanaifanya. Ni kazi itakayokupatia furaha na ridhiko la kweli kila uifanyapo au uonapo wengine wanaifanya. Tusiogope sana vitisho vya dini zetu kwani dini zetu nyingi nazo zimevamiwa na watu ambao hawakupaswa kuziongoza na ndiyo maana vitisho vya kuingia motoni vinaongelewa zaidi kuliko uhakika, usalama na amani ya kuingia mbinguni (kiimani zaidi)
Niwakati wa kuitafuta na kuitumikia kazi iliyotuleta duniani. Sisi kama binadamu ni lazima tuwe na utu, upendo na amani ili tuweze kuheshimiana na kusaidiana vyema na kuishi maisha ya ukweli na uhalisia kuliko ya kufoji yenye mateso na lawama tele.
Ebu kila uamkapo asubuhi jipangie ni kazi gani utafanya na ni ipi unayoipenda na jioni kabla ya kulala angalia ni kwa kiasi gani umeitenda kazi hiyo na kujipongeza hata kama ujaimalizia kwa kujihaidi kuimaliza tena. Furaha ya kweliitaanzia hapo na malengo ya kweli na ya msingi utayatengeneza na hiyo itakuwa ni hatua nzuri ya kuwa na malengo nakubwa zaidi yatakayofanya kipato chako kuongezaka.
Tutafute sababu ya kuumbwa ketu na kuikamilisha. Tujenge moyo wa kujiamini kwani tukijidharau tutadharariwa ila tukijiamini, tutaaminika na kuishi vyema. Eti wewe ungependa ukishakufa (kwani ipo siku uataondoka tu) au ukiacha kazi yako au uwanasiasa wako, ukumbukwe kwa lipi? Tuhuma, uzembe, majungu unafiki au kusaidiana, heshima, umoja malengo nk? Kwa nini usikumbukwe kwa jambo zuri la kusaidia jamii? Unadhani akina Nyerere walifanya nini zaidi ya kuitumikia jamii kwa moyo, uadilifu, umoja na malengo?
Rudi kwenye kazi iliyokuleta duniani bwana.

3 comments:

Bwaya said...

Kaka ujumbe huu murua sana. Ndicho kitu ambacho mie hujikuta nikikijadili niwapo na wenzangu.


Kanuni ni kujitambua. Watu wengi hatujajifahamu. Tunawafahamu watu wengine hata tunaweza kuthubutu kuwajadili. Tunafahamu mambo mengi yasiyoweza kutusaidia kwa sababu ha-tu-ji-e-le-wi.

Namaanisha self-concept kutia msisitizo. Matokeo yake kila tunachofanya tunajenga juu ya mchanga. Tunasoma tusichokijua. Tunafanya kazi tusizozipenda. Tunaiga. Tunaishi maisha ya wengine. Tumezaliwa halisi, lakini twafa as copies (natia ladha kidogo samahani). Kwa hiyo unakuta mzunguko wa maisha yetu ni makosa matupu. Kwa sababu hatukutumia muda wa kutosha kujifahamu nafsi zetu.

Bila 1 sifuri zote zinazofuata ni upupu hata kama zingekuwa mia moja.

munale said...

Kujitambua ni kazi pevu ndo maana watu
wanashindwa,mathalani maprofesa wengi wa
Africa hawajitambui.

Anonymous said...

Ni kweli kabisa ni wachache sana "wanaishi kwenye nyumba zao" wanaojua kusudi la kuja duniani. Lakini kwa kupitia mijadala kama hii inaweza kuanza kuwafungua watu hatimaye kujua kusudi la kuwepo duniani. Ingawa katika dini mbali mbali zinasema tumekuja kumuabudu Mungu. Kuabudu maana yake ni kutoa upendo au kutenda mema. Lakini jee ndicho kinachofanyika kweli? Kwa nini? Inawezekana ni uelewa wetu mdogo au kuna maarifa zaidi yanahitajika. Naunga mkono asilimia mia moja maoni ya wachangiaji juu ya kanunu ya kujitambua.