Friday, September 18, 2009

Ni wangapi wanaoweza kuridhika?

Maisha yetu ni yale yale ya kukimbizana na kukimbilia kilicho mbali siku zote. Tunatamani mishahara mikubwa, vyeo vikubwa, wenza wa aina fulani fulani. Tunatamani na kuishi kwa utashi zaidi wala sio kwa mapenzi ya kweli na uhalisia kiasi kwamba dunia inatisha si siku zote tunaogopa tu.

Ukiwa na waliokuzunguka, hamkosi kutofautiana, ukiwa peke yako, ndani mwako kuna kelele na vurugu kibao. Unatamani kuwasha redio, kusoma kitabu, gazeti au hata msaafu. Au unatoka ili utembeetembee, mambo yanaboa, duh.

Sasa maisha yanaaza kukutishia. Ni magumu, huwezi kukaa peke yako, unatamani uwe na wengine, ukiwa nao, hamkawaii kukosana na kugombana. Na hii ndio sababu familia nyingi zina migogoro. Tunaona makosa kiurahisi kuliko mazuri au hata kusahihishana. Maisha ni ya masharti kweli kweli.

Tunatafuta mali na kujitahidi kumiliki mali nyiiingi zaidi ili tuumiliki ulimwengu na kuna wanaojiaminisha kuwa wanamiliki ulimnwengu kumbe ni mateso matupu. Unafikiri marais na wabunge wana amani yoyote na kuona maana halisi ya maisha? Hawana. Wanatawaliwa na hofu, huzuni ni kuhangaika ili waendelee kuwa madarakani.

Tunakufa kwa presha kwa sababu ya kutaka kumiliki kitu fulani na tunasahanu kwamba kuna kitu muhimu tunachokimiliki ambacho ndicho cha kujivuna nacho kuliko vinginevyovyote viwavyo. Kitu hicho ni sisi wenyewe. Hakuna awezaye kutumiliki sisi isipokuwa sisi wenyewe tunajimiliki. Badala yake tunakimbizana na vile vya nje yetu tukidhani vitatupa furaha kumbe furaha ya kweli imo ndani mwetu.

Ninapopanga kuanza maisha mapya kwa kurudi kijijini, nafikiri itanisaidia sana kuliko kuendelea kutafuta nisichokihitaji hapa mjini. Utafutaji huo kamwe hauwezi kufanikiwa kwani nikipata hiki, natamani kikubwa zaidi kama wewe vile. Kumbe vitu vichache tu vinanitosha na hivyo naweza kuishi bila stress kule vijijini kuliko kuhangaika na kufukuzana mijini.

Au unasemaje wewe. Unadhani ipo siku utaridhika? Hapana na kwa hiyo ni lazima utafanya kazi mpaka uvunjike, utaamua kuiba na kuwa fisadi kwa kuamini utapata furaha na utaishia kufa kwa hofu na ugiligili kwani kamwe hatokipata kile unachokitafuta nje yako, labda urudi ndani mwako ndimo kilimo humo.

AMINA

4 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Kuridhika! Kwa haya maisha niliyoishi sijawahi kuona watu wanaridhika na kitu chochote kila na sijaelewa kabisa kwa nini?
Kila siku tunaona watu wasivyoridhika kuanzia kimwili, chakula, nguo au tuseme maisha kwa ujumla. Hata wengine hawaridhiki na asili yao. Kazi kwelikweli.

Mzee wa Changamoto said...

Mpaka pale tutakapojipa nafasi tunayostahili katika nafsi zetu na kuacha kuyatanguliza maisha basi hatutang'ang'ania kutafuta ridhiko la mali, hatutaogopa mwili na hatutaumiza miili yetu kwa kazi za ajabu na matendo yasiyo na manufaa ya mwili. Tukiacha kugombea ufahari wa kumili vitu vingi, ufahari wa kufanya mapenzi na watu wengi, ufahari wa kuwa mahala panapoheshimika na kuogopwa na wengi, uyfahari wa kuwa na idadi ya watembelwaji wengi kuliko uwezo wetu wa kuwaelimisha ama UFAHARI WA AINA YOYOTE UNAOTANGULIZA MALI NA SI MWILI, basi tunaishia kutafuka ridhiko tusilolijua.
Asante saaana kwa maelezo mema.
Natamani wengi wangeweza kusoma na kutafakari kisha kuwekeza katika UNDANI wa kilichozungumzwa hapa.
Blessings

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

Amen

Chacha Wambura said...

habari ndo hiyo.

sina la kusema mkuu kwani umigonga penyewe hapo kabisaa.

ila hujatwambia ni kijiji gani unahamia...je ni cha Maisha plus?