Monday, October 5, 2009

maisha yetu na... makala katika kwanza jamii

Maisha yetu ni yale yale ya kukimbizana na kukimbilia kilicho mbali siku zote. Tunatamani mishahara mikubwa, vyeo vikubwa, wenza wa aina fulani fulani. Tunatamani na kuishi kwa utashi zaidi wala sio kwa mapenzi ya kweli na uhalisia kiasi kwamba dunia inatisha sisi siku zote tunaogopa tu.

Ukiwa na waliokuzunguka, hamkosi kutofautiana, ukiwa peke yako, ndani mwako kuna kelele na vurugu nyingi. Unatamani kufungulia redio, kusoma kitabu, gazeti au hata msaafu. Au unatoka ili utembeetembee nakadhalika.

Sasa maisha yanaaza kukutishia. Ni magumu, huwezi kukaa peke yako, unatamani uwe na wengine, ukiwa nao, hamkawii kukosana na kugombana. Na hii ndio sababu familia nyingi zina migogoro. Tunaona makosa kiurahisi kuliko mazuri au hata kusahihishana. Maisha ni ya masharti kweli kweli.

Tunatafuta mali na kujitahidi kumiliki mali nyingi zaidi ili tuumiliki ulimwengu na kuna wanaojiaminisha kuwa wanamiliki ulimwengu kumbe ni mateso matupu. Unafikiri marais na wabunge na wengi wa wennye utajiri mkubwa wana amani yoyote na kuona maana halisi ya maisha? Hawana. Wanatawaliwa na hofu, huzuni ni kuhangaika ili waendelee kuwa madarakani na sio kutumika wala kutumikia kama inavyopaswa.

Tunakufa kwa presha kwa sababu ya kutaka kumiliki kitu fulani na tunasahau kwamba kuna kitu muhimu tunachokimiliki ambacho ndicho cha kujivuna nacho kuliko vinginevyovyote viwavyo. Kitu hicho ni sisi wenyewe. Hakuna awezaye kutumiliki sisi isipokuwa sisi wenyewe tunajimiliki. Badala yake tunakimbizana na vile vya nje yetu tukidhani vitatupa furaha kumbe furaha ya kweli imo ndani mwetu.

Nilikutana na binti mmoja ambaye ni mhitimu wa chuo kikuu cha Dar es salaam. Binti huyo aliniambia kuwa anafanya kazi fulani ya kuingiza takwimu katika tarakishi. Nilimpongeza na kumtakia mema lakini yeye hakutaka na wala hataki hayo mema niliyomtakia kwani alinieleza kuwa akipata kazi kwingine anawezakuachana na kazi ile kwa sababu eti haimuhakikishia ¨future¨ au maisha ya baadaye

maisha ya baadaye maanake nini nini? Anafikiri mshahala anaolipwa hautoshi. Anatamani mshahala zaidi. Ndivyo ilivyo katika maisha ya jamii yetu na kwa walio wengi. Hatufanyi kazi kwa bidii wala kwa malengo fulani, bali tunatafuta vyeo, tunatamani pesa zaidi ya tunazolipwa sasa na tunatamani kumiliki mali nyingi zaidi ya tulizonazo sasa.

Katika ofisi za umma kwa mfano, naibu katibu mkuu anatamani kuwa naibu waziri, huku katibu mkuu akitamani kuwa waziri na waziri anatamani kuwa waziri mkuu au rais. Ndivyo ilivyo, na rais anatumia kila mbinu kuhakikisha anaedelea kuwa rais na furaha ni kwamba hapa Tanzania hatujapata rais wa kubadili katiba ili afie madarakani kama zilivyo nchi nyingine kama Uganda , Libya au Zimbabwe .

Tamaa za vyeo na mali ndizo zinazotuzuia kuishi kwa malengo na badala yake tunatamani nakuamua kuwa mafisadi. Tunaipenda na kuitumikia miili yetu utadhani haitakuja siku tulazimike kuiacha (kufa). Tamaa hizo ndizo zinazotupeleaka jela, kuishi kwa hofu, wasi wasi na mamjuto.

Mmoja kati ya maafisa wa benki kuu walioko rumande kwa tuhuma za ufisadi, ni mkristo mzuri na mzee wa kanisa mojawapo la KKKT jijini Dar esalaam. Wazee kama huyo ndio walioko mstari wambele katika mambo ya kanisa. Wanaonekana kumjua Mungu kuliko wengine na sasa maandiko ya biblia yanaanza kuwageuka kama lile lisemalo yaliyofanyiwa gizani yataanikwa nuruni. Ulokole wao sasa wanatamani kuukana hukuwaumini wenzao waliobaki nyuma wakijaribu kuwaombea kwa Mungu asiyekuwa fisadi. Kwa nini wanawaombea? Labda hawawaombei wale walioko rumande, wanajiombea kwani wanajua kesho yaweza kuwa wao.

Tunajitengezea wenyewe jamii ya vurugu iliyojaa visa na visasasi, yenye kushitakiana na kukwaruzana. Hatujikagui ndani mwetu, tunalalamika tu muda wote na kuwalaumu wengine. Ikifika zamu yetu tunaona kama tunaonewa. Kumbe wale tunaowalaumu sio wao bali tunaona ishara ya mabaya yetu kupitia wao. Tunakila haja ya kujitambua na kujua nafasi yetu katika jamii badala ya kuishi kwa tamaa na kuongozwa na hisia.

Sisi kama binadamu ni lazima tujue kazi iliyotuleata duniani na kuitumikia vyema badala ya kutanga tanga. Matatizo yanayoikumba jamii yetu kwa kiasi kikubwa ni kwasababu wengi wetu hatuajaamua kuisaidia jamii na badala yake tumekamatwa na tamaa ya kutoridhika tukabakia kuwa wa kukimbiza kilicho mbali yetu na kug├íng´ania tulicho nacho. Sio wa kutumia tulichokwisha kuwa nacho na badala yake tumeendelea kufukuza cha mbali na kulimbikiza hata tusichokihitaji.

Tunashindwa kujua kuwa kila kitu ipo siku tutakiacha. Dini zetu nazo zinasisitiza waumini wake kukusanya pesa nyingi kwa njia za matoleo mbali mbali badala ya kuwakuza kiroho kama kazi kuu na ya msingi ya dini hizi na labda ndio sababu mafisadi wanakumbatiwa katika nyumba za ibada kuliko wasiokuwa mafisadi ambao hawana pesa nyingi za kutoa na labda tusema masikini.

Masha yetu yameedelea kuwa ya kujisifia jinsi tulivyosoma, tunavyojua lugha za kigeni, tunavyokula vyakula vizuri, ulevi na hata umaarufu. Vyombo vyetu vya habari vimejaa habari za kushtusha pekee na kutishiana utadhani hamna mambo muhimu ya kuelimisha wananchi. Vimekuwa ni vya kuandika na kutangaza habari zisizonamuhimu eti kwa sababu tu zinalipa.

Tunahitaji jamii bora. Jamii inayoishi kwa malengo, jamii iliyojitambua. Tusipoweza kupunguza tamaa, wakati utafika na sasa upo karibu ambapo ufisadi na vitendo viovu vitageuzwa kuwa halali. Bila kujitambua na kuishi kwa uhalisia, maisha yetu yatakuwa ni kazi bure. Kipi muhimu kati ya kuishi kwa mshikamano,umoja utu, kufanya kazi kwa bidii kwa faida ya wengi na kuishi kwa ubinafsi, uchoyo na tamaa?

Si kila mtu alikufa au atakufa? Kipi bora kati ya kujilimbikizia mali ili uishi kwa wasi wasi, hofu au kuwa mlinzi wa mali hizo na kuishi maisha mema yenye malengo na nia za kweli? Kwa nini tunasoma? Ili tutagatange tukitafuta mali zaidi mpaka tuishie kuwa wezi, mafisadi na matapeli au tuisaidie jamii yetu hata sisi wenyewe kwa kula jasho letu na halali yetu?

Kwa nini tusiishi kwa upendo na kueneza upendo? Kwa nini tunaendelea kuwa na viongozi wanatumia kila njia ili waweviongozi badala ya kuwa na wale wa kuombwa na hata kulazimishwa kuwa viongozi wakijua kwamba uongozi ni kazi nzito inayohitaji kujitoa kuwatumikia wengine?

Kujitambua sisi wenyewe kwanza ili tuweze kuitambua nafasi yetu ni muhimu. Katika maisha yetu tunajua mambo mengi, tunatenda mambo mengi. Tunajua jiografia ya dunia nzima, tunajua sayansi, tunajua aina za vyakula, wanyama na hata nchi na tunatenda katika mkabala huo. Lakini ajabu ni kwamba tunajua kidogo sana au hatujui chochote kuhusu sisi wenyewe – hatujitambui. Maarifa ya kujitafuta na kujigundua ili tujijue sisi wenyewe ndiyo ya msingi kwanza.

Mashuleni na vyuoni tunaandaliwa ili kuwa wazalishaji bora lakini hatufundishwi kuhusu sisi. Ndio maana tunaishia katika tamaa za ufisadi. Tunashindwa kutambua hata chakula stahiki kwa ajili ya miili yetu na hivyo kula hovyo mpaka tunapata magonjwa. Kujua kuhusu sisi au kujitambua ndio msingi. Ni lazima tujijue kwanza ili tuweze kujitedea mema. Bila kujitendea wema sisi wenyewe hatuwezi kuwatendea wema wengine, itakuwa ni ndoto ya mchana

wengi wa watu waliokwisha kuiacha miili (kufa) na kuendelea kukumbukwa walijitahidi kwa kiasi kikubwa kutenda mema, kuwa wema na kuishi kwa faida ya jamii pana. Sio kuwa mafisadi wa kujilimbikizia mali tu. Katika suala la mali tuelewane. Kumiliki mali nyingi sio kubaya, kibaya ni tamaa na kujilimbikizia hovyo hovyo hadi kuishi kwa hofu na kuikosesha jamii mahitaji yake ya msingi.

Amani ya kweli na upendo wa kweli vimo ndani mwetu. Nilazima tuweze kujitambua kwanza na kuishi kiuhalisia ili tuweze kuepuka tamaa, mihemko na vuruu zisizokuwa za lazima. Ni lazima tuyaishi maisha kwa uhalisia badala ya mateso kuishi kwa kugushi na kwa kujikataa. Hata kama unaamini kuna mbingu, kumbuka huwezi kwenda na kufarahia maisha ya huko kama hujaweza kwanza kuyaishi maisha ya hapa ambayotayari uko nayo. Maisha yoyote yajayo yawe ya mbinguni / ahera au hapa duniani, yanategemea yale uliyonayo sasa. Yaishi haya kwanza, jitambue ili ujiheshimu

4 comments:

Chacha Wambura said...

hapo patamu saaaana!!!

ni ujumbe murua kabisaa!

Yasinta Ngonyani said...

nakunukuu"Kujitambua sisi wenyewe kwanza ili tuweze kuitambua nafasi yetu ni muhimu. Katika maisha yetu tunajua mambo mengi, tunatenda mambo mengi. Tunajua jiografia ya dunia nzima, tunajua sayansi, tunajua aina za vyakula, wanyama na hata nchi na tunatenda katika mkabala huo. Lakini ajabu ni kwamba tunajua kidogo sana au hatujui chochote kuhusu sisi wenyewe – hatujitambui. Maarifa ya kujitafuta na kujigundua ili tujijue sisi wenyewe ndiyo ya msingi kwanza." mwisho wa kunukuu. Hapa umenena kwanza jitambue mwenyewe ili uweze kuitambua nafsi yako safi sanma nimelipenda somo la leo.

Mzee wa Changamoto said...

Ahaaaaa!!
Nimekupata

Markus Mpangala said...

haswaaaa kaka! basi ni hivi kwa kikoloni nami niongeze. WHEN YOU CAN LIVE FOREVER, WHAT DO YOU LIVE FOR?