Monday, December 14, 2009

Tuengeneze Nyerere wa kizazi cha leo.

makala hii ilitoka katika gazeti la kwanza jamii......

Naandika makala juu ya Nyerere kwa kuchelewa kutuokana na kuwa kwangu vijijini wakati wa siku ya kumbu kumbu ya kifa cha Mwalimu Julius K Nyerere. Siku hizi kijijini kwetu kuna umeme hata kama ni mbali, kuna huduma za kompyuta nakadhalika lakini sikuwa kwenye mazingira ya kuweza kuandika makala na tutaliona hili kiutambuzi kwamba ni kwanini kuna wakati tunapawa kuwa mbali na kelele na shughuli zetu za kawaida na kuingia katika mazingira mapya.

Katika kukumbuka siku ya kifo cha mwalimu Nyerere, nilibahatika kusoma magazeti kadhaa na kusikiliza vyombo vya habari juu ya maoni ya watu mbali nbali kuhusu maisha ya Nyerere na tathmini ya miaka kumi ya kifo chake. Wengi wetu wanaonekana kutokujua hitaji letu halisi haswa sisi kama kizazi cha leo juu ya Nyerere na maisha yake.

Wengi wanaongelea maisha ya Nyerere na kifo chake kama suala la kidini zaidi. Wanatamani Nyerere arudi, wanashindwa kujua kuwa Nyerere hawezi kurudi kamwe, muda wake kuondoka ulifika na akaondoka na nyakati zake ziliisha pita pia. Hata mchora katuni mmoja alichora katuni ya Nyerere akiwa amerudi na anawatandika viboko baadhi ya watu walioenda kinyume na maadili au matakwa yake

Wengi wa waandishi wa makala na watoa maoni wanamfananisha Nyerere na Yesu Krisito (anayeaminika kuwa muasisi wa dini ya ukristo). Inasemekana kuwa Yesu Kristo atarudi siku moja kuwakomesha watenda maovu. Hivyo ndivyo wengi wanavyomchukulia Nyerere kuwa labda anaweza kurudi. Wanashindwa kujua ya kwamba Nyerere na Nyakati zake haziwezi kurudi. Wanadhani Nyerere akirudi atatenda yale aliyoyatenda. Wanashindwa kujua kuwa hata kama angerudi hizi sio Nyakati zake na hivyo ni nyakati za kizazi cha sasa kujenga jamii bora, imara na endelevu.

Tunapotamani na kutegemea kuwa labda Nyerere anaweza kurudi tunajinyanyasa na kuwapatia nafasi wadhalimu waendelee kutudhalilisha. Hizi ni nyakati za kutengeneza akina Nyerere wapya wa kizazi chetu na wamazingira yetu. Ni kweli tunamengi ya kujifunza, kuiga na kufuata katika maisha ya hayati Nyerere lakini pia tunahitaji wakombozi wetu wa kizazi cha leo na sio kuendelea kutarajia kurudi tena kwa hayati Julius K Nyerere.

Swali lingekuwa; Nyerere alifanya nafasi yake kwa wakati wake, lakini je sisi tunaomlilia na kulalama, tumefanya nini na tunafanya nini katika nafasi zetu na Nyakati zetu ili kuikomboa jamii yetu? Hivi kweli nafasi yetu ni kumlilia tu Nyerere au ni kuwa watu bora na kujenga jamii bora?

Kwa nini tusitengeneze akina Nyerere wapya wa kizazi cha leo badala ya kumlilia tu Nyerere aliyepita na kutuamani arudi wakati hawezi kurudi? Kwanini magazeti yetu yasijae kurasa zenye maisha ya Nyerere na utafiti juu ya nini kilimfanya Nyerere afinikiwe kutenda Mema mengi aliyoitendea jamii yetu ili tuone njia badala ya kuota ndoto za mchana kuwa atarudi?

Koero Mkundi ni binti mdogo anayeammini kuwa Nyerere hajafa. Anadai hajafa kwa kuangalia matendo yake, maandishi yake nk. Ni kweli hajafa. Kifikra, kiroho na hata kiutu bado tuko naye, tunamuua sisi wenyewe kwa kutarajia arudi wakati yupo. Tunashindwa kumhishi na kuwawezesha wengine na hasa vijana wadogo wamhishi na badala yake tunasaidiana kulia lia.

Tutengeneze Nyerere wapya na wa kizazi chetu watakaoyaishi na kuyaendeleza mema ya hayati baba wa taifa na kuzaa jamii inayotenda mema.

2 comments:

Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti! said...

tusaidie kabla hatujajisaidia...lol

Masangu Matondo Nzuzullima said...

Yesu aliwaachia wanafunzi wake kazi ya kuendeleza uYesu wake - na walifanya hivyo.

Nyerere pia nafikiri alihakikisha kwamba anamwachia mtu kazi ya kuendeleza uNyerere wake (kuna mtu alikwenda kumpigania kule Chimwaga mwaka 1995). Kulitokea nini?

Kama kawaida, makala nzuri na yenye kufikirisha!