Monday, April 12, 2010

maoni juu ya waandishi wetu na uwezo mdogo

Wengi wanapinga vikari maoni ya rais Mstaafu wa awamu ya tatu Benjamini W. Mkapa juu ya maoni yake kuwa waandishi wa habari wa Tanzania wana uwezo mdogo. Labda wengi wao wanapinga ukweli, wanaukataa ukweli, hawataki kujua kuwa ili mtu ajue ni lazima atambue kwanza ni wapi kutokujua kwake kulipo yaani utakapo jua kuwa hujui ndipo utakapo jua kama alivyosema mwanafalsafa mmoja wa ugiriki ya kale
Lakini ni ukweli mtupu kwamba waandishi wetu hawana taarifa za kutosha, au wahabarishaji wetu hawana habari za kutosha. Ukisikiliza waandishi wa kiTanzania kwenye mahojiano na viongozi wetu, unashangazwa sana na masuala na maswali wanayoibua, ni mambo yasiyokuwa na umuhimu, unagundua kuwa hawana taarifa za kutosha juu ya wakifanyacho.
Ni rahisi kwa Mtu kama Benjamin Mkapa kukereka kwa kuongea na watu kama hawa. Juma lililopita nilikuwa kwenye basi na hivyo kujikuta nikisikiliza mahojiano na redio moja iliyokuwa ikimhoji mtaalamu wa masuala ya mazingira juu ya athari Tanzania izipatazo kutokana na mabadiliko ya tabia nchi. Inashangaza maswali ya mwandishi / mtangazaji Yule. Wakati Tanzania sasa inakumbana na hatari kubwa ya mabadiliko hayo, Yule mwandishi alikuwa akihoji juu ya viwanda vilivyojengwa kwenye makazi ya watu kule mbagala na kwingineko, vituo vya mafuta katika makazi ya watu nk
Yaani mwandishi kama huyo siyo kwamba tu hana taarifa za kutafuta kwa kusoma juu ya atahari hizi, bali hata zile zainazojionyesha hadhalani kama vile ukame ulipita, mafuriko ya kule Morogoro, mvua za hatari za hivi karibuni jijini Mwanza, vimbunga vya mkoni Kagera, mvua za kule Arusha, mbeya nk
Sasa unaagalia mwandishi kama huyu, kwa nini asiwekero kwa mtaalamu aliyekuja kuongelea athari za mabadiliko ya tabia nchi zinazoonekana na kufahamika kirahisi na za kitaalamu zaidi? Mambo kama ya viwanda ndani ya makazi ya watu ni madogo na yanamalizika kiurahisi kuliko jinamizi hili litujialo japo mwandishi / mhabarishaji hana habari la mabadiliko ya tabia nchi
Hii inaendana na wamiliki wa vyombo vya habari pamoja na waandishi tunaowaita mavetereni. Angalia magazeti yetu na vyombo vyetu vya habari na habari vizitoavyo. Kwa mfano, gazeti la Raia mwema nilisomalo kila juma, nimeona makala mbili tu mahususi kwenye matoleo ya hivi karibuni yanayoongelea juu ya mabadiliko ya tabia nchi na hili ni gazeti linaloandikwa na waandishi wakongwe waliobobea katika fani ya uandishi
Vyombo vya habari viko bize na propaganda za kisiasa zisiizosaidia lolote. Zinaandika habari mshutuso tu (shocking news) badala ya kuandika vitu vya kumjenga msomaji akabadili maisha yake badala ya kubakia kuilamu serikali. Wamiliki na waandishi wa vyombo vyetu hivi baadaye wakishika nafasi za kiutawala hamna mabadiliko yoyote ya msingi waletayo. Kwa hiyo hulalamika kama wivu wao kwa walioko madalakani au ili waonekane wanavyojua kuandika (naomba nisitoe mfano wa waadishi kama hawa ambao sasa wako madarakani nakutenda zaidi ya waliolalamikia enzi zao sasa wanayatenda hayo kulikoilivyokuwa)
Angalia makala zijaazo gazeti kama raia mwema na mengine, ni za kisiasa, zisizomwezesha msomaji kufanya mabadiliko. Lazima nikubali kuwa kuna waandishi makini wanaokuja na vitu vya tofauti na vinavyojenga. Waandishi kama Karugendo, Mihangwa na hata Lula. Hujaribu kuonyeha mambo muhimu ambayo hata yakishindwa kuleta mabadiliko, basi huchangamsha bongo za msomaji
Lakini vitu muhimu hakuna. Tungekuwa na waandishi makini katika taifa lenye njaa japo lina ardhi kubwa na nzuri, vyanzo vya maji na hata mvua za kutosha kulima, lingetuonyesha ni kwanini waTanzania wana njaa na wafanyeje kujiokoa na njaa na kunufaika kiuchumi, lakini hubakia kulalamiki serikali, au vingetuonyesha ni kwa kiasi gani ukosefu wa walimu kwenye shule za kata, ungepunguzwa kama kila mTanzania mwenye elimu angetoa muda wa masaa mawili kwa juma kufundisha shule iliyoko karibu naye au hata wanavyuo na wafanyakazi waendao likizo, wangetenga muda wao mfupi kufundisha shule hizo, hakuna, tunaonyeshwa ubaya wa serikali tu
Utafiti uko mwingi. Ukisikiliza vyomba vya habari vya nje ambavyo Mkapa alivisifia kwa wanahabari mahiri, utashangaa kuona vinaongelea mambo ya ndani ambayo yalipaswa kuongelwa na vyombo vyetu lakini hakuna. Kwa mfano hidhaa yakiswahili ya BBC London au hata gazeti la the East African. Unashangaa jinsi vilivyomakani kiasi kwamba hata mtu akivisoma anapata taarifa kamili inayoweza kuleta tofauti au mabadiliko kwake
Nivigumu kwa maoni kama haya yasemayo ukweli kupata nafasi ya kuchapisha magazetini na utakuwa muujiza ukiyasoma kwani daima sisi hatukosei na hutupendi kukosolewa, tunajifanya tunajua huku tukiungua jua! Hakuna ajuaye kupita sisi. hii ndiyo kanuni ya waandishi na wahariri wetu asiowapenda mkapa.
Vyombo vya habari kama wavihitavyo mhimiri wanne, lazima viwe vya kuhabarisha watu na kuleta tofauti sio kufanya hata mambo yasiyo mabaya kuwa mabaya. Kila jambo au tukio lina pande mbili ubaya na mzuri. Ni lazima tuwe na vyombo vya habari vya kuweza kutuonyesha tufanye nini kutumia jambo lionekanalo baya kupata zuri tulipendalo, hili litaletwa na waandishi na wahariri makini ambao sio lazima wawe wasomi / waliokaririshwa vitu tu darasani, wasioandika kwa ujuaji bali kwa moyo wa kupenda kupokea maoni ya wengine
Inashangaza niadikapo makala kama hizi hukataliwa na vyombo vya habari vya ndani kama gazeti la raia mwema lakini hupokelewa na kukubaliwa na vyombo vya habari vya nje nikiandika kwa lugha ya kiingereza. Ndio maana natamani mtandao ya internet uenee nchi nzima na wananchi wengi wawe na uwezo wa kusoma magazeti tandao (blogs) mtandaoni ambao mwandishi yuko huru kusema atakacho na aonavyo badala ya kukumbana na urasimu wa waadishi wetu wenye mtizamo hasi kwa kila kitu na wanye vipaumbele vya ajabu ajabu katika kazi zao.
Ni lazima tuukubali ukweli huu wa mzee Mkapa ili iwe hatua ya kugeuka, kujifunza na kubadilika.
Kamala J Lutatinisibwa
jlkamala@yahoo.com
kamalaluta.blogspot.com
0754 771 601
0715 771 601

3 comments:

Masangu Matondo Nzuzullima said...
This comment has been removed by the author.
Masangu Matondo Nzuzullima said...

Uchungu ulionao unasikika vyema; na sababu zilezile ambazo zilifanya gazeti letu la Kwanza Jamii likafa umezigusia.

Zamani nilikuwa nayalaumu sana magazeti ya udaku lakini sasa nimebadili msimamo. Kama habari zinazoandikwa na magazeti haya yanayojiita makini ni zile zile kila uchao, mbona watu wasikimbilie kusoma juu ya bosi kufumaniwa laivu au Rubagumya kubambwa akila denda na Mwanaisha uchorochoroni?

Magazeti mengi yanaendeshwa kisiasa na nadhani ndiyo maana ni vigumu sana makala zenye mwelekeo mpya wenye kuamsha watu kukubaliwa. Watu wakijitambua ni hatari ati! Unataka wanaume hawa wajifunge kengele wenyewe?

Lakini pia inabidi tulitazame tatizo hili katika upana wake. Elimu yetu ni mbovu mno na kusema kweli pengine hatuna hata haki ya kuwalaumu hawa waandishi wa habari. Watakuwaje makini wakati elimu waliyopitia ni ile tunayoijua? Wamefundishwa katika lugha wasiyoifahamu. Wamefundishwa na waalimu waliopata D mbili, waalimu ambao wenyewe wanaishi katika maisha magumu sana. Wamesoma kwa kukariri katika shule ambazo hazina vitabu wala maabara. Wamesomea katika utamaduni ambamo mtu ukiuliza swali unaonekana kuwa adui na unaweza kuambulia viboko. Ni haki kweli eti leo ndiyo tuwategemee kuwa watabadilika kwa kuwa tu eti wamekuwa waandishi wa habari? Hili si tatizo la waandishi wa habari. Ni tatizo la jamii nzima na nimesikitika kwamba Mkapa hakuliona hili wakati alipokuwa madarakani na kulishughulikia. Ni sekta gani ambako hakuna ubabaishaji? Ni wapi ambako hakuna uzembe ambao mwingine unatokana na watu kutojua wanachopaswa kukifanya. Elimu-kombozi ndiyo mkakati mama katika maendeleo yetu na bila kuleta mabadiliko ya kweli katika mfumo wetu wa elimu daima tutabakia kuzunguka jangwani tu na mwishowe sote tutafia humo. Pengine Haruni mpya ataibuka huko mbele, Haruni atakayekuwa na nia ya dhati ya kutufikisha katika nchi ya ahadi (kama ipo!)

Kamala, gazeti la Jitambue (kama sikosei) lililokuwa linachapisha makala nyingi za Marehemu Munga Tehenan liko wapi? Mliliachia likafa? Pengine wewe, Kaluse na watambuzi wengine itabidi muunganishe nguvu mlipiganie au muanzishe jingine. Hapa Marekani mambo ya utambuzi yanavutia watu wengi sasa na nadhani hata huko nyumbani sasa watu wameanza kutambua umuhimu wake.

Vinginevyo tuacheni sie tuendelee kuburudika na Risasi, Amani, Sani, Uwazi na mengineyo

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

unachokisema uko sawa, gazeti la jitambue lina mgogoro kidogo ila ishu ni nani atakuwa mhariri kwani sisi sote hakuna hata mmoja aliyesomea uandishi wa habari na kuwatumia wahariri wa kawaida ni changamoto

mimi naishi mikoani na hiyo inaongeza changamoto zaidi ila na tuone itakavyokuwa kwani hata mimi naamini utambuzi ni muhimu zaidi na zaidi au ikibidi waadishi na wahariri woote wapewa maarifa haya