Wednesday, September 15, 2010

nimetumiwa Email hii kuhusu dr Slaa....

SOMA KWA UMAKINI

Mtanzania yeyote Mzalendo wa kweli, mwenye akili timamu, asiye na mtindio wa ubongo, wala mtumwa wa hila chafu, wala udumavu wa kiakili, tena asiye na utando wa buibui wala tongotongo za ufisadi machoni, wala asiye mzembe wa kufikiri, anaalikwa asome kwa uangalifu na azingatie makala hii na awashirikishe ndugu, jamaa na marafiki zake popote pale walipo..Dr Slaa yes we can! Huyu ni mtanzania wa pili baada ya Nyerere kuchukia ufisadi kwa vitendo. Ni mtanzania wa pili kuchukia umaskini wa watanzania kwa vitendo. Ni Dr. Slaa aliyesimama na kutaja majina ya wala rushwa na mafisadi. Akataka wale wanaopinga wampeleke mahakamani. Hakuna aliyethubutu kujitokeza kumpeleka mahakamani.Ni Dr. Slaa aliyesimama bungeni kuomba posho za wabunge kupungzwa kuzielekeza zaidi kwa watanzania maskini. Ni Dr Slaa aliyesimama bila woga kunyosha vidole kwa matumizi mabaya ya ofisi za umma. Ni Dr Slaa amekuwa mtanzania baada ya Nyerere kutoa hoja za nguvu zinazomlenga kumkomboa mtanzania maskini. Maisha bora kwa kila mtanzania yako wapi? Ajira milioni moja ziko wapi? Hebu mwenye mbavu za kujibu swali hili ajibu bila unafiki!Ni Dr Slaa anayeweza kudhibiti matumizi mabaya ya ofisi za umma. Ni Dr Slaa anayeweza kuwapa elimu ya bure watoto wetu pale mlimani. Achana na longolongo za CCM kuwatoza ushuru watoto. Waulizeni majukwaani wao Nyerere aliwatoza ada? Kama si kutaka watanzania waendelee kuwa mambumbumbu ni nini? kama si kutaka watanzania tuendeleee kuwa watumwa ni nini? Ni Dr. Slaa anayeongelea treni ya umeme kwenda Kigoma, Dodoma, Tabora, na Mwanza. Waulize mpango wao ccm kama si kuwapa wahindi wanaoleta mabehewa ambayo mababu zetu walitumia wakati wa ukoloni. Sasa wahindi wanabaki kutudanganya na bajaji wakati vyuma chakavu vya reli sasa vinatumika kujenga vyoo. Hawa hawatutakii mema. Hawana tofauti na akina Carl Peters.Ni Dr Slaa anayeongelea mfumko wa bei -nani hajajua dola leo hii ni sawa na tsh 1500. Uchumi unadidimia kwa kasi. Ahadi nyingine za uongo lukuki zinatolewa tena, wakati zile tulizoahidiwa mwaka 2005, hata moja haijatekelezwa. Watanzania walio wengi na hasa wa vijijini, wamelala usingizi. Wanafumbuliwa macho, lakini wamesinzia bado! Wanatabasamu, wanachekelea na kuridhika na vitisheti vya kijani na vikofia za njano. Wamekwishazoea shida kiasi kwamba wanadhani ni sehemu ya maisha yao. Ee mwenyezi Mungu, tunusuru na hili balaa..Ni Dr.Slaa anaweza kuzuia wizi wa matrilion ya pesa kutoka migodi yetu ya Buzwagi, Geita, Bulyankulu, Buhemba, Nyamongo, Tulawaka, Nzega na Tanzanite. CCM wameshindwa kwa sababu ni washirka wakubwa na wameruhusu wizi huo. Ni Dr Slaa anaeweza kuwalipa wafanyakazi zaidi ya shilingi 350.000 achana na CCM ambayo imeshindwa kusimamia maliasili ambazo zingeliwapa wafanyakazi kima cha chini kinachokidhi mahitaji yao.Ni Dr.Slaa anayeweza kusimamia mashirika ya umma kuleta tija achana na CCM wanaofyonza michango yetu kule, kwani haya mashirika yameshindwa nini kuwajengea nyumba wanachama wake? Mbona kwingine yameweza? Ni Dr.Slaa anayeweza kuongoza nchi bila woga, kwa utawala wa kweli wa sheria bila kuwaonea watu wala bila kulipiza visasi.Ni Dr. Slaa ambaye amepanga kubadili katiba ili Rais afuate matakwa ya walio mwajiri ambao ni wananchi. Waulize CCM hata kama mtu kaiba anapewa mda arudishe pesa. Hivi inaingia akilini kweli? Utawala wa sheria uko wapi? Naomba niwape heko ITV kwa kuturejeshe kwenye hotuba za mwalimu. Katika hotuba yake moja alisema waziri mmoja kule uingereza aliandikwa kidogo tu gazetini juu ya kashfa, yule waziri alijiuzulu na waziri mkuu hata hakumjibu bali aliteua mtu mwingine.CCM hawawezi hayo? Eti wanataka ushahidi. Nani kawambia rushwa tule wawili harafu tutoe vielelezo? Tunaiona rushwa kwa matokeo yake. Matengenezo ya barabara ya bilion 200, baada ya siku mbili imeharibika. Kwanini usimfukuze waziri na katibu wake wa wizara kwanza? CCM hawawezi! eti wanataka vielelezo! Ni Dr Slaa anayeweza kufanya hayo. Si tumeona mnazi mmoja alivyowataja mafisadi wote! hapo akiwa ni mbunge tu! Je akiwa rais si watakimbia nchi? Jamani nawambia tumpe miaka mitano tu awakurupushe muone moto utakavyowaka.. Tutapata dawa, tutapata shule za bure, tutapata madawati. Jamani hivi kweli karne ya leo watoto wanasoma wamekaa chini? we must be serious! Hivi kweli dunia ya leo watu wanavuliwa nguo njiani kwenda Mwanza, Shinyanaga, Tabora, Kigoma, Mbeya, Lindi na Mtwara kwa sababu ya usafiri wa malori? Nani asiye jua madaktari wetu wengi bingwa wapo botswana kwa sababu ya maisha duni Tanzania na hivi kwenda kutafuta maisha bora wakati hapa kwetu wananchi maskini wanakufa bila madawa? Nani asiyejua matatizo ya umeme, maji, makazi, maradhi, yanavyotutesa? Nani asiyejua wakulima wetu wasivyokuwa na masoko ya mazao yao? Nani asiejua asilimia 85 ya watanzania wanatumia vibatari au makoroboi kama mwanga? nani asiejua tunavyonyonywa na hawa wakoloni waliokuja kuchukua kila kitu?? Jamani wafanyakazi, wakulima, na wanafunzi, kwa nini mnalala usingizi? Kwa nini mnapiga miayo ya njaa wakati maghala yetu yamejaa nafaka? Ni akili gani hii? Nchi yetu inazo raslimali za kututosha, lakini wanaozifaidi ni vibaka wachache. Mtalala hadi lini?Ni Dr Slaa mzalendo wa kweli, na sio kwa ajili ya sifa, anaweza kutuvusha tulipo. Nchi hii ni maskini na umaskini wenyewe ni wa kujitakia. Tanzania ni tajiri tuna kila kitu - mito, maziwa, national parks, migodi, mazao ya misitu, na kila aina ya utajiri. Lakini tuko maskini wa kutupwa! Naona huruma na umaskini wa kifikra wa watanzania.Hivi kuna mtu hajui mapolisi wanalala kwenye vibanda vya mabati? Hivi kuna ambao hawajui mapolisi watendaji wanalipwa laki moja? Wamekosa nini hawa? Ni ajabu! pamoja na laki yao moja utakuta bado wanatumika kuwanyanyasa watetezi wao. Hata maaskari amkeni hiyo laki moja yenu haina tija hadi mrubuniwe kuwanyanyasa wapinzani ambao kimsingi wanawatetea ninyi! Hivi maaskari mnayo macho ya kuona? Jamani tuache woga inawezekana! Mbona Kenya wameweza? Mbona malawi wameweza?Mbona zimbabwe wameweza? Mbona Ghana wameweza? Kufanya mabadiliko sahihi, inawezakana na nafasi ni hii tuitumie. Tumtume Dr Slaa atukurupushie wezi wote na atuwekee katiba sawa. Huo ndio msingi wa yote. Ni Dr. Slaa asiyeogopa kuwepo na mgombea binafsi. CCM hili hawaliwezi. Wamelipinga hadi mahakamani. Wanataka wao tu ndio waendelee kututawala na kutunyonya. Jamani 2010 hakuna kudanganyika! enough is enough. Acheni kudanganyika. Wakati ndio huu. Watanzania msipoamua sasa, mtamlaumu nani tena? Nawatamani watu wa kule Mara -hakuna kura inaibiwa. Zote zinasimamiwa. Tukibadilika inawezekana, tena ni rahisi. Peleke ujumbe huu kwa marafiki, ndugu, jamaa, babu na bibi yako kule kijiji ambako wanadhani bado Nyerere ndiye rais wa nchi hii. Peleka ujumbe huu haraka kwa simu kama ipo, au kwa njia ya posta, mradi tu wale jamaa waliochoka kuishi wasiikwapue barua wakidhani ni hela..
Quote

10 comments:

Fadhy Mtanga said...

yes we can

Anonymous said...

Uchaguzi Mkuu wowote katika nchi yeyote ile unajijenga juu ya cafetaria ya agenda.

Kung'ang'ania ajenda moja tu ni sawa na referendum!

Labda CHADEMA, kama wana akili, waitumie ajenda ya UFISADI iliyozimwa Bungeni, kama referendum ya kuitoa CCM madarakani!

emu-three said...

Sifa zake ni ndeefu, na tunajua kila mgombea sasa hivi ana sifa ndeeeefu, cha msingi ni kukaa na kutafakari, bila kujali rangi, dini au kabila, angalia nini unataraji na nani ataweza kulifanikisha hilo tarajio lako , na taifa lako...wamesema mengi na watasema mengi, mwisho wa siku ni kura yako tu , itaamua!

Albert Paul said...

Mabadiliko ya watawala na chama tawala ni muhimu kwa maendeleo yetu.

Masangu Matondo Nzuzullima said...

Nina wasiwasi sana na "ukombozi" huu wa kutegemea "masihi" mmoja. Watu wamesahau kwamba alikuweko mtu mmoja akiitwa Mrema (na NCCR Mageuzi ya akina Mabere Marando na Makongoro Nyerere) ambaye alikuwa akibebwa na gari lake kusukumwa kila alikoenda. Sijui leo yuko wapi.

Halafu akaja Mchungaji Mtikila na siasa zake za magabacholi. Moto ukawaka, watu wakavua mashati, mioyo ikadunda na midundiko ikachezwa. Sijui leo yuko wapi.

Halafu wakaja ngangari wa CUF na Lipumba wao na Maalim. Nao jua lao likachomoza, hiloooo tukaliona, saa sita ikaingia na hatimaye jioni yao ikafika. Leo hii Lipumba yupo kama hayupo.

Asubuhi ya Dr. Slaa ndiyo hii imeshafika. Mimi hata hivyo sina matumaini sana kwa sababu mabadiliko tunayohitaji ni ya kimfumo hasa na siyo ya kutegemea mtu mmoja mchapakazi mwenye bashasha. Siwajui sana Chadema lakini sijui kama Dr. Slaa ana wafuasi wa kweli wanaoamini kile anachokiamini kwa asilimia 100. Historia inatuonyesha kwamba bila wafuasi wa kweli, ni vigumu sana kwa mtu mmoja kuleta mabadiliko ya kweli katika jamii. Kamuulize Nyerere atakwambia. Yeye alikuwa akiimba Ujamaa na Kujitegemea wakati wenzake waliomzunguka wakijibeparisha (Rejea hapa: http://matondo.blogspot.com/2009/10/mwalimu-nyerere-na-jangwa-lake-la.html)

Japo email ya huyu mdau - ambayo imeenea mtandaoni - inamchora Dr. Slaa kama Musa wetu - bila wafuasi wa kweli na mshikamano wa dhati na umma ni kazi bure. Na mashabiki wake inabidi wawe tayari kuyakabili maluweluwe yatakayowapata baada ya uchaguzi. Na baada ya uchaguzi huu naamini wataanza kutafuta nyota nyingine inayong'ara zaidi. Natumaini pengine atakuwa Mh. Zitto.

Mabadiliko yameanza kutokea lakini ni ya polepole na mimi naamini kwamba bado safari ni ndefu kidogo kwa wapinzani kuweza kukifikia kilele. Ili kufikia azma hiyo inabidi wasiwe tu wanasubiri wakati wa uchaguzi ndipo wanakurupuka kutoka usingizini huku wakiweka matumaini yao yote kwa "Musa" mmoja tu mshika kurunzi! Ukombozi wa kweli wa wanyonge ni kazi ya wote na ni kazi ya masaa yote 24, kutokea Jumatatu mpaka Jumapili; na mwezi wa kwanza mpaka wa kumi na mbili wa KILA mwaka!!!

Anonymous said...

Huyu aliyetuma msg hajui watu tunaangalia nini kwa sasa pamoja kuwa CHADEMA wana sela nzuri lakini ukabila ni mwingi katika bunge lilopita wanawake viti maakum wato walitoka wote ni wachaga kasoro mmoja ailiyetoka kigoma.

Katika safu ya uongozi Mwalizilishi ni Mtei ambaye amewahi kuwa mwenyekiti lakini alipotoka yeye aliingia msukuma ambaye ni Bob Makani ambaye alikuwa ni shemeji yake na Mtei alipotoka Makani alipewa Mbowe ambaye ni Mkwe wa Mtei ukiangalia jinsi uongozi unavyokwenda CHADEMA ni chama cha wanafamilia.

Tunahitaji chama kisichokuwa na wabaguzi , wakabila na ndo maana CCM wanashinda kwa sababu CCM ni wote

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

@matondo, naamini daima tunahitaji mtu mmoja wa kwanza wa kuongoza au wa kushika tochi na wengine watafuatia tu, siamini kama ni Slaa pekee, wapo wengi hata wengine ndani ya CCM na vyama vingine ambao ni wakombozi wa kweli lakini kwa sasa ni zamu ya DR slaa kuongoza mashambulizi

binafsi sina upande kivyama ila napenda tanzania iliyo bora kwa wote


wewe Anony kuna vitu viwili umesahau kwamba labda hata wabunge woote wa chadema ni wachagga, lakini pia hata mchaga anasifa za kuikomboa nchi kama ataona ni yeye na wachaga wenzake wanaoweza kuikomboa tanzania

ila sasa CCM nayo ni ya masikini au??

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

@matondo, naamini daima tunahitaji mtu mmoja wa kwanza wa kuongoza au wa kushika tochi na wengine watafuatia tu, siamini kama ni Slaa pekee, wapo wengi hata wengine ndani ya CCM na vyama vingine ambao ni wakombozi wa kweli lakini kwa sasa ni zamu ya DR slaa kuongoza mashambulizi

binafsi sina upande kivyama ila napenda tanzania iliyo bora kwa wote


wewe Anony kuna vitu viwili umesahau kwamba labda hata wabunge woote wa chadema ni wachagga, lakini pia hata mchaga anasifa za kuikomboa nchi kama ataona ni yeye na wachaga wenzake wanaoweza kuikomboa tanzania

ila sasa CCM nayo ni ya masikini au??

John Mwaipopo said...

kama wachagga ni watu wabaya basi tusiende kwenye baa zao, tusinunue nguo zao kariakoo, tusinunue kitimoto wanayotengeneza vizuri kwa ubunifu (nenda B-Bar Sinza ukaonje, au kule kigogo).

kama wachagga ni wabaya basi tusinunue vifaa vya ujenzi kutoka ktk maduka yao. nk nk nk nk

hivi kumbe slaa ni mchagga?

Mzee wa Changamoto said...

Bado siamini maamuzi ya Dr Slaa kugombea uRais. Nadhani angezunguka nchi nzima akipiga kampezi za watu kuchagua wabunge wa upinzani.
Hivi hawa wana nini kwenye ngazi ya KAYA ambacho tunaweza kujivunia kuwa wakipata madaraka WATAFANIKISHA utekelezaji wa sera walizonazo?
Kwani hata SLAA AKISHINDA LEO WAKATI 90% YA WABUNGE NI WANA-CCM, UNADHANI ATAMUADHIBU NANI? ATATUMIA KURA GANI AMA SHERIA GANI ISIYOPITA BUNGENI KUWAADHIBU ALIOSEMA WANAIIBIA SERIKALI?
Pengine ni wakati wa sasa watu kutambua kuwa tunahitaji miaka 5 ijayo kujijenga katika ngazi muhimu za chini kabla ya kuanza omba ngazi za juu.
Hivi nchi hata iongozwe na MASIA anayetawala ki-demokrasia, unadhani itafanikiwa kama asilimia 98 ya watendaji ni WAPINZANI WAKE tena wasiopenda kuona anafanikiwa?
Nadhani Slaa anachotakiwa kufanya ni kukubali kushindwa kisha kutumia misingi waliyojenga kuzunguka nchini bila kuchoka kujenga ngazi za chini.
Japo hili haliwezekani kirahisi kwa kuwa uchaguzi hautafanyika mpaka miaka 5 ijayo. Nilitamani kama ungekuwa unafanyika miaka 2.5 ijayo kama nilivyandika (http://changamotoyetu.blogspot.com/2009/07/nionavyo-mimi-uchaguzi-wa-rais-na.html)
Uchaguzi ungekuwa unafanyika katikati ya muhula, Slaa na wenzake wangeendelea na kampeni kwa miaka 2.5 kisha kuhakikisha wabunge na watendaji wa kata wanabadilika kisha "wamchachafye" rais kuhakikisha anatekeleza ahadi na kama anakamilisha ahadi vema zikawa zinapingwa na wabunge, apelekewe wabunge watakaoms-sapoti ili kuwafaa wananchi.