Thursday, January 6, 2011

katiba tuliyonayo ni zao la Nyerere na unyerere wake

katika Afrika mashariki tuna viongozi wawili maarufu, hawa ni maarufu zaidi hapa Tanzania na kule Uganda. vyombo vya habari na hata mtaani huongelewa sana kila mtu kwa upande wake. Viongozi hawa ni yule wa Tanzania mwl J.k.Nyerere na mganda Idd Amin dadah

litamkwapo jina la Idd Amin hufuatwa na vicheko na matusi ya kutosha. alikuwa dictator, gaidi, mla watu, mbakaji na hata huitwa jina la kimaasai 'nduli' yaani makalio!

lakini litamkwapo jina la Nyerere huenda na sifa lukuki kama vile baba wa taifa (utadhani alihudhuria mkutano wa berlin ulioizaa tanganyika), mjamaa mkombozi, mpigania uhuru/haki, mkulima na sasa mtakatifu /mwenyeheri!

naamini (na ni kweli) kuwa pamoja na ubaya wake Idd amin alikuwa na mazuri yake pia na hata Nyerere alikuwa na mabaya yake na huu ndio ubinadamu, huwezi kuwa na upande mbaya tu au mzuri tu

kwa waliosoma katiba hii unaweza kushangaa ni kwa nini kiongozi mwenye sifa lukuki kama Nyerere alipitisha katiba hii! katiba hii pia ilikuwa haihojiwi kwa kipindi kirefu na sasa imekuja kuhojiwa (labda na kuwa hadharani) miaka mingi baada ya Nyerere kufa! hii ikiwa na maana kwamba kwanza katiba ilikuwa siri (kwa wanaoelewa maana ya katiba itashangaza inakuwaje siri) lakini pia katiba hahiojiki!

ukiisoma katiba hii vizuri utamuelewa Nyerere halisi kuwa alikuwa mtu na mtawala wa namna gani! wapo wanaomtunzia siri eti kwa wakati ule ilikuwa sahihi, siamini kama kuna wakati ambao iliwahu kuwa sahihi kwa katiba kuwa siri dhidi ya wenye nayo (wananchi) au kutokuwa na mamlaka ya kuihoji!

tuangalia maajabu ya nguvu za rais kwenye katiba yetu then tujaribu kuitofautuisha na ukoloni ili tumjue Nyerere halisi!

Lutatinisibwa

11 comments:

emu-three said...

Hakuna kizuri kisicha na kasoro. Nayakumbuka sana haya maneno, yalionyesha wazi nini kilichokuwepo:
ZIDUMU FIKIRA ZA MWENYEKITI
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
Hii zidumu, ...ina maana ni msahafu...
Ndio maana hata mimi nasema hakuna chema kisichokuwa na kasoro na huenda ilikuwa hivyo ili iwezekane wakati huo, lakini wakati huu basi...TWAHITAJI MABADILIKO, YA WENGI, SIO FIKIRA ZA MMOJA, SIO CHAMA KIMOJA,...

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Wapo watakaomtetea kwamba alifanya hivyo kulingana na mazingira ya wakati ule. Tulikuwa tu ndiyo tunajipatia uhuru (kama kweli tulipata uhuru!) na Nyerere na "mababa" wenzake wa mataifa kote barani Afrika walijibebesha madaraka yote kwa kisingizio kwamba walihitaji mamlaka kamili ili kunyosha mambo mpaka mataifa yao yatakapotengemaa na kusimama dede. Huku wakisaidiwa na "ujinga" wa wananchi wao, haukupita muda wengi wa "mababa" hawa waligeuka kuwa miungu watu, wakaendelea kukakawana madarakani na kuhakikisha kwamba mawazo yao na falsafa zao pekee ndiyo zinatawala. Nyerere naye anaingia katika kundi hili ingawa pengine hakuwafikia wenzake akina Mobutu, Bokassa, Amin na wengineo. Unazikumbuka Imani na Ahadi za Mwana TANU? Katiba ya TANU je? Zidumu Fikra SAHIHI? Nyerere alipiga propaganda nzuri sana kuhakikisha kwamba mawazo yake na "uungu" wake unakubalika.

Kinachomtenganisha Nyerere na wenzake wengi, hata hivyo, ni jinsi alivyoishi na alichojaribu kufanya hasa siasa zake nyingi zilizoshindwa. Kutokujilimbikizia mali kwake kumekuja kutazamwa kama kielelezo kizuri kwamba kumbe aliamini kabisa katika falsafa zake za Ujamaa na Kujitegemea alizokuwa akizihubiri. Pia kitendo chake cha kuachia madaraka kwa hiari kilikuwa (na bado) cha nadra sana kwa viongozi wengi wa bara hili. Na ni lazima tukiri kwamba alikuwa na bashasha, msomi na mtu mwenye welewa wa mambo wa kiasi cha juu sana, jambo ambalo lilimfanya aheshimiwe duniani kote.

Ni kweli katiba hii inayopigiwa makelele sasa ni matokeo ya sera zake. Mazingira sasa yamebadilika na ndiyo maana inatakiwa kufanyiwa marekebisho.

NB: Nakumbuka tulipokuwa darasa la nne tulishinda juani siku nzima tukiimba nyimbo za CCM huku tukimsubiri afike. Mpaka jioni tukiwa hoi ndiyo tukatawanywa na kuambiwa kwamba alikuwa amechelewa na hataweza kufika siku hiyo. Mpaka leo nazikumbuka nyimbo zile za kusifia Mwongozo wa CCM, Madaraka vijijini, Vijiji vya Ujamaa, Azimio, Ahadi na Sifa za Mwana CCM na bila kusahau Fikra Sahihi za Mwenyekiti wa Chama. Tumetoka mbali ati!!!

Wachumi said...
This comment has been removed by the author.
Wachumi said...

Poleni,ilibidi niirudie kwani nilichemsha.

Nilikua nimesema kwamba...Kumbaka lakini kwamba,ingawaje katiba yake "unyerere" ilimpa nguvu kubwa sana kiutawala Nyerere hakuchukua kwa "granted" sapoti kwa wananchi maana kila baada ya miaka mitano alikwenda kuomba kura. Iddi Amini huyo,na wengine wengi, hawakufanya na walitumia nguvu na kinga za kikatiba kujinifaisha na kuwatesa wananchi.

Ni muhimu tunapomkosea marehemu Mwalimu tuweke sawa na wazi yote ambayo sio tuu aliyoyafanya bali hakuyafanya. Angekua na roho mbaya katiba hiyo ingemruhusu kufanya chochote alichokitaka. Lazma tuheshimu heshima aliyotupa sisi watanzania kwakutujali kama binadamu na ndugu zake,na sio "watawaliwa" tu (ingawaje chama chake,na yeye pia,kili/kinatutawala.

Mbele said...

Wa-Tanzania hawasomi maandishi ya Nyerere. Kadiri siku zinavyopita, elimu yao kuhusu Nyerere wanaipata huko vijiweni, baa, na kitimoto. Huko hawachambui maandishi na hotuba za Nyerere. Ni majungu tu kuhusu Nyerere ndio yanayotamba huko.

Kuna hasara kubwa zinazotokana na kutosoma maandishi ya Nyerere. Ingekuwa wanasoma maandishi ya Nyerere, hawangekuwa wanaipigia kura CCM, kwa jinsi Mwalimu alivyoichambua katika maandishi yake, kama vile "Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania."

Mwalimu Nyerere alichangia kuanzisha TANU, chama ambacho muda wote kilikuwa kinajitahidi kutetea maslahi ya wananchi, kuanzia kupigania uhuru hadi kupambana na mfumo wa kibepari wa kimataifa. Azimio la Arusha ilikuwa ni sehemu ya mapambano hayo.

Hata kama TANU haikufanikisha malengo yake, kama lengo la Ujamaa na Kujitegemea, moyo wake wa kujitahidi ninaushangilia.

Mwalimu Nyerere alichangia kuanzisha CCM kwa imani kuwa ingeendeleza haya mapinduzi. Lakini haikupita muda alitambua kuwa CCM imetekwa nyara na wahuni. Hayo unayasoma katika maandishi ya Mwalimu Nyerere na katika hotuba zake za miaka ya themanini na kitu na tisini na kitu.

Sio sahihi kumhusisha Nyerere na hii CCM ya leo, ambayo ni rafiki wa mafisadi. Na hao CCM na mafisadi wenyewe hutawasikia wakitaja haya maandishi ya Nyerere ninanyoongelea.

CCM hii inastawi kwa sababu ya umbumbumbu miongoni mwa wa-Tanzania. Wa-Tanzania kwa vile hawasomi vitabu vya Nyerere, wanaendelea kuamini propaganda za CCM kwamba CCM ni warithi wa Mwalimu Nyerere.

Tangu tulipopata Uhuru, Mwalimu Nyerere alitutahadharisha kuhusu adui ujinga, maradhi, na umaskini. Leo hii wa-Tanzania wameukumbatia ujinga. Na kutokana na huu ujinga wa wa-Tanzania, CCM inaendelea kukamua. Na bado; CCM itakamua hadi hapo wa-Tanzania watakapopata akili, maana wajinga ndio waliwao.

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

@matondo! ni kweli labda aliachia madaraka japo kuwa naona kama alig'atuku kwani alikuwa hana jipya. kama asingeachia madaraka angeumbuka vibaya na labda ndio maana CCM na Tz kwa ujumla vikaanza kupotea vibaya sana baada ya Nyerere kuachia madaraka!
kama asemavyo mbele , waTZ hawasomi lakini hata hivyo Nyerere hakupenda kubishiwa na ndio maana alibakia kufuatwa na watu wasio na uwezo mzuri wa kufikiri na akakosa mtu mwenye fikra sahihi wa kurith uongozi! angalia wana CCM wakongwe woote, hamna hata mmoja anayekemea ujinga!

chib said...

Ni asilimia moja tu ya watanzania ndio wameshawahi kuiona katiba, hii haijumuishi wangapi wameisoma ingawa wameikwishaiona

Goodman Manyanya Phiri said...

Ndugu Kamala

Nasoma blogi yako mara ya kwanza baada ya kukufahamu pitia blogi ya mama mmoja Yasinta Ngonyani.

Nimependa sana jinsi akili yako inavyoonekana kali au SHARP (unisamehe kama Kiswahili dhaifu, mwenzio Mwafrika Kusini aliyejifunza Kiswahili mitaani ya Dar na Morogoro tu).

Posti hii imenikuna kwasababu katiba ya kila nchi ni karatasi tu iliyechafuliwa na wino; na mwananchi yoyote yule anaweza akazidisha ule uchafu wake kwa matumizi chooni... lakini ole wake yule pamoja na majirani zake!

Katiba inahitaji kila mwananchi aliyekuwa nayo asome, ajadili na kama inamridhisha atetee kilichokuwa mule. Moja yake katika uwanja wa mapambano makubwa juu ya katiba ni kortini za nchi. Kwa sisi Waafrika Kusini tumebahatika kuwa na katiba inayoturidhisha, lakini ukweli ni kwamba wananchi huku kwetu wako chooni nayo zaidi kuliko kwenye meza au darasani... bado tunanyanyaswa na Wazungu vilevile umezuka ukabila waakina Nelson Mandela na kabila lake Wathembu lakini tunapigana kortini kutetea vipengele vya usawa waMswahili na bindadamu yoyote mkazi waAfrika Kusini.

Hata hivyo, mie nafikiri siku iko karibu tutakuwa na nchi moja na serikali moja barani Afrika.

Hongera Bwana kwa posti hii tena!

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

asante bwana phiri kwa somo kwamba kumbe hata katiba mpya inaweza isiwe suruhu kama tunavyofikiria japo ni hatua.

tuzidi kuwasiliana ili kuelimishana

Goodman Manyanya Phiri said...

Nakweli, Ndugu yangu, tuwasiliane daima! Tena nitatazama ile posti yako kama sikosei kuhusu pikipiki ili kuchunguza kama kweli umekwisha nunua ule mkokoteni badala ya ile pikipiki yakukuangusha, pole tena!

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

duh sawa bwana phiri, ni mkokoteni tu na sio pikipiki tena maana ajali ya mkokoteni ni bora kuliko ya pikipiki