Saturday, May 4, 2013

Munga Tehenani, bado tunakukumbuka

Ilikuwa ni tarehe tano mwezi wa nane mwaka 2008 ndipo gwiji la utambuzi na Mahusiano ndugu Munga Tehenan alipoachana na mwili wake wengine wanasema kufa. Nilimfahamu Munga miaka miwili kabla ya kifo chake. Allijitolea kunisaidia bure kunfundisha masuala ya saikolojia, imani pamoja na utambuzi ili niweze kujitambua.

Kama kijana nilifika njia panda na kushindwa kuiona njia, nikadondokea mikononi mwa huyu bwana. Mimi na wenzangu wengi tulijifunza mengi juu ya sisi ni nani, maisha ni nini, imani na hata  masuala ya uchumi na fedha. 

Munga alitufundisha kwa unyenyekevu na kwa moyo mkubwa bila kuchoka na wala kudai malipo ya fedha kutoka kwetu ni moyo wa ajabu sana maana hata kanisani wahubiri hudai sadaka. Alifundisha juu ya ndoa na tendo la ndoa na hivyo kusababisha amani kubwa kwenye ndoa zilizokuwa njia panda.
Aliniwezesha kuzikabili changamoto za kifamilia na jinsi ya kuhishi na watu mbali mbali na pia jinsi ya kupata utulivu na uzingativu kupitia tahajudi/meditation ambako niliweza kujua tofauti kati ya miili minne aliyonayo  mwanadamu na hata tofauti iliyopo kati ya mtu na mwili wake. Darasa lake daima lilianza kwa Swali la mimi ni nani/nini?

Mwishoni mwa mwezi wanne mwaka 2008 Munga aliugua maradhi ya moyo yasiyoelezeka vizuri na baadae akalazwa katika hospitali ya Hindu Mandal ya jijini Dar. Munga hakuogopa kifo, nilienda kumjulia khali hospitalini akanambia ya kuwa kama asingepelekwa hospitalini hapo, basi angeisha achana na mwili wake.

Niliporudi hosipitalini kumuona tena, aliniambia ya kuwa anafikiria kuachana na mwili (kufa) kwa kuwa ugonjwa ulimsumbua mno na hivyo yuko tayari kufa. Asubuhi ya tarehe tano mei nikiwa naelekea kumjulia khali, nilipigiwa simu na rafiki yangu McDonald na kunipasha habari za kifo cha Munga Tehenan, nilishtuka na kuwahi hospital kushuhudia mwenyewe.

Nilipofika chumbani alimokuwa, nilikuta mwili wake ukiwa umefunikwa na kufungwa kwenye shuka jeupe mzima mzima na mwanafunzi wake mwingine akiwa nje huku akibubujikwa na machozi. Nilijizuia kulia kwani Munga alitufundisha pamoja na mambo mengine kuzoea kifo. Basi kwa kushirikiana na wafanyakazi wa Hindu Mandal, tuliubeba mwili wake na kuuhifadhi mortuary na kesho yake tukauzika rasmi kwenye makaburi ya Kisutu jijini Dar.

Munga aliacha mjane na watoto watatu na pia aliacha darasa zuri la utambuzi linalozidi kushamiri mpaka sasa. Namshukuru kwa moyo wake wa kutoa bure elimu ambayo kimsingi ni ya gharama kubwa sana 

Kamala Lutatinisibwa

2 comments:

katawa said...

kwa tuliobahatika kufundishwa na Munga,tumebahatika kurahisisha maisha kwa kukabiliana na changamoto.

Anonymous said...

Ni kweli kabisa, Munga alikuwa gwiji la utambuzi na atakumbukwa daima!